Marion Lalisse, mratibu wa kupambana na uhalifu wa chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) katika Tume ya Ulaya, akizungumza kwenye mkutano wa diplomasia mjini Antalya, Uturuki, alieleza kuwa tangu kuanza kwa vita hivyo tarehe 7 Oktoba 2023, uhalifu unaochochewa na chuki dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani umeongezeka kwa asilimia 140. Alionya kwamba: "Bila shaka, vitendo hivi ni hatari kwa Ulaya na havilingani na maadili ambayo Umoja wa Ulaya umejengwa juu yake."
Ingawa chuki dhidi ya Uislamu si jambo jipya barani Ulaya, imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, hasa wakati wa vita vya Gaza, katika mataifa kama Ujerumani na Ufaransa. Hali hii inaonesha kuwa chuki hiyo haichochewi tu na misimamo ya kibinafsi, bali imejikita kwenye sera za kisiasa, hali ya kijamii, na mitazamo ya kitambulisho. Kwa mfano, kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu kufuatia mabadiliko ya kisiasa na kijiografia, kama vile vita vya Gaza, kunaonesha wazi kuwa chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya umejikita kwenye hali halisi ya kijamii na kisiasa. Kawthar Najib, mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Liverpool, anasema: "Kauli za kuunga mkono Israel kutoka kwa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, wakati wa mauaji ya Gaza zimezidisha waziwazi ubaguzi wa kimfumo dhidi ya Waislamu."
Waislamu barani Ulaya wamekuwa wakikabiliwa na mawimbi ya vurugu na mashinikizo. Kuzorota kwa hali ya kisiasa na kiuchumi barani humo kutokana na mzozo wa Ukraine, ongezeko la wakimbizi, na sasa vita vya Gaza, kumeifanya hali kuwa mbaya zaidi kwa Waislamu.
Pia, ongezeko la ushawishi wa vyama vya siasa za mrengo wa kulia katika nchi nyingi za Ulaya kumechangia kwa kiasi kikubwa. Vyama hivi, ambavyo mara nyingi huwa na misimamo mikali ya kupinga uhamiaji, hutumia kampeni zao kueneza hofu dhidi ya Uislamu na kuahidi kuwafukuza wahamiaji. Mfano mmoja ni chama chenye misimamo mikali cha Alternative for Germany (AfD), ambacho kiliingia bungeni kwa kutumia kaulimbiu za kupinga Uislamu. Tangu wakati huo, mashambulio dhidi ya misikiti na ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu vimeongezeka kwa kasi.
Katika Ufaransa, hali ni hiyo hiyo. Sheria za kupiga marufuku hijabu mashuleni na baadaye katika taasisi za serikali, kufungwa kwa baadhi ya misikiti, na kuvunjwa kwa taasisi za Kiislamu ni ishara kwamba madai ya Ufaransa kuwa mtetezi wa haki za binadamu hayana mashiko kivitendo.
Vyombo vya habari, kampeni za uchaguzi za vyama vya siasa za mrengo mkali wa kulia, na mgawanyiko wa jamii vimechangia pakubwa kuendeleza hali ya kutoaminiana na chuki dhidi ya Waislamu. Farid Hafez, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha William & Mary, anaeleza kuwa vyama hivi vimegeuza chuki dhidi ya Uislamu kuwa njia ya kunufaika kisiasa, jambo linalochochea ubaguzi wa kisiasa na wa kimfumo dhidi ya Waislamu.
Kwa kifupi, kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya, hasa tangu kuanza kwa vita vya Gaza, kunaonesha wazi undumakuwili au unafiki wa msimamo wa Ulaya. Wakati Umoja wa Ulaya unasisitiza maadili ya demokrasia, haki za binadamu, na uhuru wa kuabudu, kwa upande mwingine unaweka sheria zinazobana uhuru huo, unaunga mkono sera za kiusalama zinazowalenga Waislamu, na unashindwa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na wimbi la chuki dhidi ya Uislamu, na kwa msingi huo, kufichua taswira halisi ya umoja huo ambayo ni kinyume na ile iliyopo kimataifa.
342/
Your Comment